Thursday, November 22, 2012

Madudu mengine Maliasili- vigogo wapora vitalu

Madudu hayo, yanatajwa kuwa pengine ni makubwa kuliko hata yale yaliyoifanya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ishauri Kamati hiyo ivunjwe kutokana na tuhuma za rushwa miongoni mwa wajumbe.

Wajumbe kadhaa wametumia mwanya wa kuugua kwa Mwenyekiti wa Kamati, Bakari Mbano, kufanya mchezo huo. Kamati hiyo iliketi kwa siku mbili - Novemba 16 na 17, mwaka huu jijini Dar es Salaam - na kutengua baadhi ya uamuzi wake wa awali wa ugawaji vitalu, na kwa mara ya kwanza, kundi la matajiri wa kigeni wenye fedha limeweza kupendekezwa kupewa vitalu vinono ambavyo viliambuliwa na kampuni chache za wazawa.

Habari za uhakika zinaonyesha kuwa kampuni zaidi ya 10 zilizopewa vitalu awali, zimenyang’anywa; kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utekelezaji wa maagizo ya Bunge ya kutaka kampuni zisizo na sifa, lakini zikapewa vitalu, zinyang’anywe.

Kwa kutumia mwanya huo, Kamati ya Ugawaji Vitalu imerejesha baadhi ya vitalu vilivyopendekezwa, lakini ikaenda mbali zaidi na kuwanyang’anya masikini wazalendo ambao walipewa vitalu hivyo baada ya kutimiza matakwa ya kisheria yaliyosimamiwa kwa ukaguzi wa kila kampuni.

Madai ya uamuzi wa kuwanyang’anya wazawa vitalu, yamefanywa kwa misingi ya rushwa na yanatokana na ukweli kwamba wanachama wa TAHOA (Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii), ambao wengi ni wageni, hawakuguswa kabisa.

Kwa namna inayoibua harufu ya rushwa, vitalu hivyo vimekabidhiwa kwa kampuni nyingine, tena za wageni, bila kufuata utaratibu wa kuvitangaza, hata kama kweli walionyang’anywa hawakuwa na sifa. Kisheria, Serikali inapotwaa vitalu inapaswa kuvitangaza ili wanaovitaka waweze kuomba.

Uamuzi wa Kamati hiyo ulifanywa chini ya uenyekiti wa muda wa Jaji mstaafu, Steven Ihema, kutokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu, Bakari Mbano, kuugua.

Wazawa kupokwa vitalu hivyo ni kutimia kwa kauli za majigambo za wageni hao walizoanza kuzitoa Desemba, mwaka jana, ukiwa ni muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya ugawaji vitalu.

Desemba 12, Waziri wa wakati huo, Ezekiel Maige, aliwaita wadau wote ofisini kwake Dar es Salaam na kuwataka wale waliopewa vitalu (vya Wazungu), waelewane kwa lengo la kumaliza migogoro.

Baadhi ya wageni hao walikuwa tayari kutoa hadi dola milioni moja (Sh zaidi ya bilioni 1.5) ili wazawa wawaachie vitalu walivyotaka. Maelekezo ya Waziri Maige yalipingwa na wadau, hatua iliyowafanya baadhi ya Wazungu hao, kwa ushirikiano na Watanzania kadhaa mawakala wao, watambe kuwa kama wamekataa fedha hizo, watahakikisha wanazitumia katika ngazi nyingine ili watwae vitalu walivyovitaka.

Endapo Waziri wa sasa wa Maliasili na Utalii atabariki mapendekezo ya Kamati ya Ugawaji Vitalu, atakuwa amekamilisha majigambo ya matajiri hao wa kigeni.

Uchunguzi wa MTANZANIA, umebaini baadhi ya kampuni zilizopewa vitalu hivyo ni za raia wa kigeni ambazo wakati wa uombaji zilijitanabahisha wazi kuwa ni za kigeni, lakini sasa zimebadili na kujitambulisha kuwa ni za Kitanzania. Mchezo huo umefanywa ili ziweze kupata vitalu na kukamilisha masharti ya kisheria yanayotaka asilimia 85 ya kampuni zinazopata vitalu, ama ziwe za Kitanzania, au wageni wawemo, lakini wakiwa na hisa chache.

Kampuni za wazalendo zimependekezwa kunyang’anywa vitalu ilhali ikiwa imesalia miezi mitatu tu zikabidhiwe umiliki wa miaka mitano. Endapo mpango huo wa kifisadi utatekelezwa, Serikali itaingia matatani kutokana na ukweli kwamba kampuni nyingi za Kitanzania zenye sifa zote kisheria zimeshapewa barua na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya shughuli za uwindaji wa kitalii.

Jaji Ihema, alipopigiwa simu jana kuzungumzia tuhuma hizo, alikataa kuingia kwenye undani wa suala hilo, kwa maelezo kwamba msemaji ni Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa. Mkurugenzi huyo naye hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, akizungumza kwa masikitiko, alisema baadhi ya Watanzania wenye sifa wamenyang’anywa vitalu na kupewa Wazungu ambao tangu awali hawakutaka kabisa vitalu hivyo wapewe Watanzania. Maeneo manono yenye wanyamapori na yanayopendwa na wawindaji wengi, yakiwamo ya Maswa, yote sasa yanamilikiwa na kampuni za kigeni, zinazopata nguvu kutoka kwa baadhi ya mawakala wao Watanzania.

Habari za uhakika zinaonyesha kuwa mmoja wa Watanzania ambaye ni mwanasheria, amehakikisha mpango wake wa muda mrefu wa kujitwalia vitalu kutoka kwa Watanzania wenzake wenye uwezo, unafanikiwa. Kuna habari kwamba mpango huo umewezekana kutokana na nguvu za kifedha na kimamlaka kutoka kwa mmoja wa watoto wa viongozi waandamizi kabisa hapa nchini.

Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii, pamoja na kutuhumiwa kukumbwa na rushwa, imeendelea kuwapo, licha ya wito kutoka kwa wabunge na watu maarufu, akiwamo aliyekuwa Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya.

Chanzo cha habari kimesema kwamba ugawaji vitalu uliofanywa wiki iliyopita uligubikwa na harufu ya rushwa, kutokana na ukweli kwamba Kamati hiyo inatambua wazi kuwa muda si mrefu itavunjwa.

“Walichoamua kukifanya baadhi ya wenzetu ni kuhakikisha kuwa wanapata pesa kutoka kwa wadau wa vitalu kwa sababu muda wao wa kuwa kwenye Kamati unahesabika,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo hicho kimesema endapo mapendekezo hayo yatatekelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kaghasheki, ni wazi kwamba atakuwa amebariki rushwa na uonevu unaofanywa na baadhi ya Watanzania kwa lengo la kuwapendelea Wazungu.

Kamati iliyovunjwa na Balozi Kagasheki, ilikuwa ikiongozwa na Bakari Mbano, ambaye amepata kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori mwaka 1995-1998.

Kamati hiyo, pamoja na Mbano na Jaji Ihema, inaundwa na Dk. Simon Mduma (Mkurugenzi Mkuu TAWIRI), Edward Msyani (kwa niaba Mkuu wa Chuo cha MWEKA) na Saidi Nzori (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali).

Wengine ni Allan Kijazi (Mkurugenzi Mkuu TANAPA), Obeid Mbangwa (Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori –ambaye alifukuzwa kazi hivi karibuni), Mbunge wa Viti Maalumu Mary Mwanjelwa (CCM), Profesa Leticia Rutashobya (Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), Daniel Nsanzugwanko (Naibu Waziri wa Kazi wa zamani), na Beno Malisa ambaye alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Wakati wa ugawaji vitalu uliofanywa awali, mgawanyiko mkubwa uliibuka ndani ya Kamati kutokana na kila upande kuvutia kwake. Hatua hiyo ilitafsiriwa kuwa ilitokana na baadhi ya wajumbe kuhongwa na wenye kampuni za uwindaji wa kitalii.

Mei, mwaka huu, aliyekuwa Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya, alizungumza na waandishi wa habari na kuishutumu Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu, akisema ilikuwa imepoteza maana na akamshauri Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki, aivunje haraka.

Alisema, “Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge na ile ya Kumshauri Waziri kuhusu Ugawaji wa Vitalu walikwishatumbukia katika mtego na kutoa ahadi kwa kampuni hizo kuwa watalitumia Bunge kugawa vitalu upya na kwamba watasaidia idadi ya kampuni hizo kupanda mpaka asilimia 30 ya uwiano (kutoka asilimia 85 kwa wazawa dhidi ya asilimia 15 kwa wageni).

“Iliandikwa katika gazeti kwamba huko Dodoma baadhi ya wabunge walikarimiwa kwa njia ya semina na mwanasheria anayetumikia baadhi ya kampuni za kigeni. Wabunge hao, kwa mujibu wa taarifa hizo, wanadaiwa walipewa posho nono ya semina hiyo.

No comments:

Post a Comment