Gazeti la Mtanzania, la kiswahili http://mtanzania.co.tz/
gazeti la Mtanzania- Wanajeshi kwa kuua raia, soma habari zaidi kwenye mtanzani
JESHI la Polisi mkoani Mbeya, linawashikilia askari 10 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa tuhuma za mauaji. Askari hao kutoka Kikosi cha 44KJ Mbalizi pamoja na walinzi wanne wa kampuni binafsi ya ulinzi ambayo haikutajwa jina, wanadaiwa kuhusika na mauaji ya mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.
Lakini hadi jana majina ya askari hao, yamehifadhiwa kwa sababu za usalama.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, aliwataja walinzi wanne wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo kuwa ni Frank Mtasimwa (25), Mure Julias (26), Omari Charles (28), wote wakazi wa DDC Mbalizi na Legnard Mwampete (30) mkazi wa Izumbwe.
Kamanda Diwani, alisema chanzo cha tukio hilo ni kulipiza kisasi kufuatia askari Godfrey Matete (30) Kikosi cha 44 Mbalizi, kupigwa na walinzi wa kilabu cha pombe za kienyeji cha DDC kilichopo Mbalizi, waliokuwa lindoni.
Alisema baada ya askari huyo kushambuliwa, alifungua kesi kituo cha Polisi Mbalizi usiku huo na kupata hati ya matibabu PF3 kwa ajili ya kwenda kupata matibabu hospitali.
Alisema baada ya Matata kujeruhiwa, siku iliyofuata watu wengine sita, walijeruhiwa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za miili yao na watu wanaodaiwa kuwa ni askari wa JWTZ.
Alisema askari hao, wanatuhumiwa kwa mauaji ya Petro Sanga (25) mkulima na mkazi wa Chapakazi.
Alisema Sanga, alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Ifisi, Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Alisema marehemu alichomwa kisu shingoni na mdomoni na kikundi cha watu wanaosadikiwa kuwa ni askari jeshi.
Alisema kundi la wanajeshi, linadaiwa kuvamia baa ya Power Night Club na kuanza kushambulia wananchi kwa kuwapiga wakitumia ngumi, mateke, mikanda, marungu, sime na mapanga.
Alisema marehemu alijaribu kuokoa uhai wake kwa kukimbia kutoka eneo hilo hadi katika grosari ya Vavene, lakini watu hao walimkimbiza hadi eneo hilo na kumjeruhi vibaya kwa kumchoma kisu.
Kamanda Diwani, alisema kati majeruhi hao, watatu walilazwa katika Hospitali Teule ya Ifisi kwa matibabu zaidi, huku wengine wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa.
Alizitaja mali zilizoharibika kuwa ni gari lenye namba za usajili T106 AWB aina ya Toyota Vista, mali ya Paulo Maximilian ambalo lilivunjwa kioo cha mbele na gari lenye namba za usajili T 884 AAU aina ya Toyota Cresta, mali ya Alile Godfrey.
Kamanda Diwani, alisema mwili wa marehemu Sanga tayari umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
No comments:
Post a Comment